Alhamisi 11 Juni 2026 - 12:15
Jumuiya ya Maulamaa wa Beirut Yapongeza Msimamo wa Dhati wa Iran katika Kuisaidia Lebanon

Hawza/ Jumuiya ya Maulamaa wa Beirut imesisitiza kwamba; haiwezekani kuachana na muqawama ambao uliikomboa ardhi na kumzuia adui; Muqawama upo na utaendelea kuwepo maadamu hakuna mbadala unaoweza kulinda na kuzuia.

Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Jumuiya ya Maulamaa wa Beirut ilisisitiza kwamba; haiwezekani kuachana na muqawama ambao uliikomboa ardhi na kumzuia adui; Muqawama upo na utaendelea kuwepo maadamu hakuna mbadala unaoweza kulinda na kuzuia.

Jumuiya hiyo, katika taarifa yake, ilieleza kwamba; Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeonesha ukweli na uaminifu katika msimamo wake wa kuisaidia na kuiunga mkono Lebanon mbele ya adui wa Kizayuni na uhalifu wake dhidi ya watu wa Lebanon wanaosimama kidete katika muqawama, pamoja na kupinga aina yoyote ya kunyenyekea au kuisalimisha ardhi na mamlaka ya nchi.

Jumuiya ya Maulamaa wa Beirut ilisema: Jamhuri ya Kiislamu imethibitisha kwamba ipo uwanjani, si katika maneno pekee, na kwamba ndiyo rafiki mwaminifu zaidi wa Lebanon ya muqawama; Lebanon ambayo haiwaachi watu wake na washirika wake peke yao mbele ya mkoloni mhalifu, Iran ilitekeleza yale ambayo ilikuwa imeahidi kwa kujibu uchokozi uliolenga eneo la Dhahiyah Kusini mwa Beirut, kupitia mashambulizi dhidi ya maeneo mengi ndani ya utawala wa Kizayuni unaokalia ardhi, ili kuthibitisha kwamba haitaiwacha Lebanon katika makubaliano yoyote yatakayoweza kufikiwa na Marekani. Pia ilifanya hivyo ili kudumisha mizania ya kukabiliana na adui Mzayuni mhalifu na kutomruhusu kufanya kila atakacho.

Aidha, Iran ilithibitisha kwamba; kipindi cha subira ya kimkakati kimefikia mwisho, na kwamba haitaruhusu Lebanon kuwa uwanja usio na ulinzi kwa adui ambaye hafahamu isipokuwa mantiki ya nguvu na haelewi chochote kingine isipokuwa lugha ya nguvu; kwa kuwa uzoefu wa makabiliano haya umeonyesha ukweli huo wazi.

Taarifa hiyo iliongeza: Sisi ndani ya Jumuiya ya Maulamaa wa Beirut, tunaishukuru na kuipongeza Jamhuri ya Kiislamu kwa kusimama pamoja na watu wetu na muqawama wetu wa kishujaa, na tunautukuza sana msimamo huu wa fahari; kwa sababu kwa vitendo imethibitisha msaada wake wa moja kwa moja na imebatilisha uzushi na kauli za uongo ambazo kwa nia mbaya zilikuwa zikieneza madai ya kinyume chake ili kupotosha, kuchochea na kuleta matumaini kwa watu wa nje.

Jumuiya ya Maulamaa wa Beirut iliendelea kusema: Haki imekuwa wazi kwa wenye akili na busara, na asubuhi imeonekana kwa macho yanayoona, na yeyote anayetaka kuendelea kukataa au kung’ang’ania upinzani wake, hilo linamhusu yeye mwenyewe, jambo muhimu kwetu ni lile tunaloliona katika uhalisia wa matukio.

Muqawama hauko peke yake, na hili ndilo ambalo viongozi wa Iran wamekuwa wakisisitiza mara kwa mara kuhusu umoja wa hatima katika medani zote za mhimili wa muqawama, mbele ya muungano wa kiburi na ubeberu ambao unajaribu kuzitenganisha medani hizo ili kuweza kuilenga kila nchi peke yake, na jambo hili, Inshaallah, halitatimia.

Jumuiya ya Maulamaa wa Beirut, pia ilitoa shukrani na pongezi zake kwa Jamhuri ya Kiislamu kwa msaada wake wa dhati kwa Lebanon ya muqawama, wakati ambao “wauzaji wa taifa” wanajaribu kunyenyekea na kujisalimisha mbele ya adui ambaye kwa muda wa miongo minane amekuwa akiifanyia Lebanon uchokozi.

Hata hivyo, katika hali kama hii, hatuwezi kuachana na muqawama ambao uliikomboa ardhi na kumzuia adui kuendeleza uchokozi wake wa asili, na maadamu hakuna mbadala unaoweza kuilinda na kuzuia, muqawama upo na utaendelea kuwepo, Inshaallah.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha